Search
Close this search box.

Kujituma, ujasiri, huruma – baadhi ya sifa za uongozi alizokuwa nazo Mhe. Benjamin William Mkapa

Share:

Uhusiano wa Taasisi ya UONGOZI na Mhe. Benjamin William Mkapa unafahamika sana kwa sababu ya nafasi yake kama Mlezi wa Kongamano la Kikanda la Viongozi wa Afrika. Mhe. Mkapa, aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alikuwa mtu aliyefanya kazi kwa bidii na kujituma sana na kwa tabia yake alikuwa mkweli. Hakuwa Mlezi kwa jina tu bali alikuwa mlezi kwa vitendo. 

Tangu mwanzo, lilipoibuka wazo la kuanzisha Kongamano, alishiriki katika kuandaa matukio akianzia kwenye kuandaa mada kuu  ya kila mwaka  kwa kuzingatia masuala muhimu katika maendeleo ya Afrika; akawahimiza viongozi wenzake wastaafu kushiriki katika Kongamano hilo, akawa mwenyekiti wa kila mkutano wa Kongomano na kushiriki kikamilifu katika mijadala ya Kongamano hilo. Alijulikana kwa udadisi wake, na licha ya kuwa mstaafu, alikuwa anajituma kweli kweli. Hakika, wafanyakazi wote wa Taasisi  ya UONGOZI walijisikia kama watu waliopendelewa sana kuwa naye.  

Kiongozi hana budi kuendana na mabadiliko ya mazingira. Kwa kawaida, jambo hili linahitaji ujasiri.  Hili ni eneo ambalo Mhe. Mkapa alidhihirisha uwezo wake waziwazi kama kiongozi. Alibaki mwaminifu kwa mafundisho ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa kwanza wa nchi yetu. Mwalimu alikuwa hasa mlezi wake kiuongozi. Mhe. Mkapa alimuenzi na mara zote  alisema mawazo ya Mwalimu yalikuwa kielelezo kwake. Lakini hakusita kuyaacha au kuyaboresha baadhi ya mawazo ya Mwalimu kulingana na mabadiliko yanayotokea kwa kasi duniani. Kufanya hivyo kulihitaji ujasiri na utayari wa kukubali mabadiliko. 

Kuelewa hisia za wengine ni sifa nyingine ya kiongozi bora. Mhe. Mkapa kamwe hakusahau shida za watu maskini na watu walio pembezoni, aliendelea kuwatetea ili wapate haki zao na thamani yao ya utu. Vilevile, aliunga mkono ushiriki wa vijana na wanawake katika maendeleo ya Tanzania. Ushiriki wake katika usuluhishi wa migogoro ya kimataifa ulidhihirisha uwezo wake wa kujali taabu za wengine. Mhe. Mkapa alikuwa muumini mkubwa wa uongozi bora. Mfano wa hivi karibuni unaoonyesha imani yake kwa uongozi bora ni pale alipotenga nafasi maalumu katika kitabu chake cha maisha yake na kutoa taarifa na ushauri kwa vijana. Ushiriki wake katika kazi za Taasisi ulianza wakati wa muhula wake wa pili kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pale wazo la kuanzisha taasisi yenye lengo la kuendeleza uongozi lilipoibuka na yeye akaliunga mkono. Hatimaye, Rais wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akaianzisha rasmi mwaka 2010.

Tukiwa tumepata heshima ya kunufaika na msaada na ushauri kutoka kwa viongozi mbalimbali wastaafu na waliopo kutoka Tanzania na sehemu mbalimbali duniani, Mhe. Mkapa alionyesha kuzipenda sana shughuli zetu tangu mwanzo na kila wakati alikuwa tayari kututia moyo na kutupa mawazo yake. Kwa sababu hiyo, sisi tunamchukulia Mhe. Mkapa kama ‘babu’ wa Taasisi yetu.

Mwaka 2019, Taasisi ilishiriki kuchapisha kitabu cha maisha yake kiitwacho: Maisha Yangu, Dhamira Yangu. Rais wa Tanzania Akumbuka (My Life, My Purpose. A Tanzanian President Remembers). Anamalizia kitabu chake kwa maneno yafuatayo:

‘Namwachia Mungu na ninyi mnihukumu kuhusu mchango nilioutoa kwa dunia hii.’

Bodi ya wakurugenzi, menejimenti na wafanyakazi wa Taasisi yetu wanashudia ukweli usiopingika kwamba Mhe. Mkapa aligusa maisha ya watu wengi. Matendo yake mema na mfanikio yake kwa Tanzania na Afrika, pamoja na mchango wake katika kuimarisha viongozi vitaendelea kuishi nasi kupitia wale ambao wameishi kwa kumtazama, na wale aliowashauri na kuwasaidia.