WAWEKEZAJI katika sekta ya uchimbaji wa rasilimali za umma wametakiwa kuwashirikisha wananchi katika maamuzi ya kutumia ardhi yao ili kuondoa migogoro baina yao.

Akifungua mjadala ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), George Simbachawene alisema kumekuwa na migogoro mikubwa katika maeneo ambayo yana uwekezaji, wananchi kushindwa kuridhishwa na uwekezaji husika.

“Tunafahamu kwamba ziko sheria mbalimbali zinazosimamia uchimbaji wa rasilimali kama madini na mafuta na mara nyingi eneo linalopatikana rasilimali hizi huambatana na fujo za wananchi kwa sababu wanakuwa hawaridhishwi na mambo yanayoendelea. Hii inatokana na kwamba hawashirikishwi vya kutosha ili wawe sehemu ya mradi”, alisema.

Aidha Simbachawene alisema wananchi wanashindwa kuridhika na uvunaji wa rasilimali kwa sababu maisha yao yanakuwa duni pamoja na uwekezaji unaokuwa ukiendelea katika maeneo yao.

“Ni lazima kuwe na kibali cha jamii katika uvunaji wa rasilimali, makubaliano ya wananchi wenyewe waone moja kwa moja faida ya uchimbaji madini au mafuta katika maeneo yao, na hii ni katika uwekezaji wote hata katika kilimo,” alisema.

Alisema hata kama kuna mikataba iliyoingiwa kati ya Serikali na wawekezaji, wananchi pia washirikishwe kuwa sehemu ya uwekezaji huo ili waone faida kwa uwazi.

Mkuu wa Idara ya Utafiti na Sera kutoka Taasisi ya Uongozi iliyoandaa mjadala huo wa siku moja, Dennis Rweyemamu alisema mjadala huo utaainisha changamoto mbalimbali kati ya wawekezaji na wananchi na namna ya kuzikabili.

Habari Leo

Link